Stori:Mwandishi wetuTaifa
linapepesuka, linayumbishwa na adui asiyeonekana, anayesababisha
kizaazaa kisha yeye kukaa pembeni akiwaacha Watanzania wao kwa wao
wakinyoosheana vidole kutuhumiana kuhusika.
IGP Saidi Mwema
Adui huyo ameivamia Tanzania na ndiye inafaa awe mtuhumiwa nambari
moja wa bomu lililolipuliwa Soweto, Arusha, katika mkutano wa hadhara wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa ufungaji wa
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Jumamosi ya wiki iliyopita.
Jinsi nchi…
Stori:Mwandishi wetuTaifa
linapepesuka, linayumbishwa na adui asiyeonekana, anayesababisha
kizaazaa kisha yeye kukaa pembeni akiwaacha Watanzania wao kwa wao
wakinyoosheana vidole kutuhumiana kuhusika.
IGP Saidi Mwema
Adui huyo ameivamia Tanzania na ndiye inafaa awe mtuhumiwa nambari
moja wa bomu lililolipuliwa Soweto, Arusha, katika mkutano wa hadhara wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa ufungaji wa
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Jumamosi ya wiki iliyopita.
Jinsi
nchi inavyopepesuka kwa sasa, ni ishara ya mafanikio ya adui huyo
ambaye lengo la uvamizi wake na harakati zake za kutibua amani ya nchi
kuona Watanzania wao kwa wao wanashikana mashati, badala ya kuzingatia
masuala muhimu yanayohitaji mshikamano wa kitaifa.

Namna
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, vinavyotuhumiana kuhusika na
ulipuaji wa bomu hilo ambalo imeshaelezwa kusababisha vifo vya watu
wanne, ni ushindi kwa adui huyo mwenye shabaha ya kutenda tukio
kiuchochezi na kuzigeuza fikra za watu kutuhumu wasiohusika.
“Tuache
kufikiria haya mambo kisiasa, tuyatafakari katika sura yenye hoja
mahususi, utaona kwamba siyo CCM wala Chadema wanaohusika na ulipuaji wa
bomu Arusha,” alisema Job Ngarano, mkazi wa Arusha, aliyejitambulisha
kuwa msomi wa shahada ya kwanza ya Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa.
NANI KALIPUA BOMU?Ripoti
ya uchunguzi wa gazeti hili, iliyokusanya taarifa za eneo la tukio na
mambo mengine ya pembeni kuhusiana na bomu la Arusha, imebaini kuwa siyo
Chadema wala CCM, mwenye uhakika na tuhuma dhidi ya mwenzake.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, alishatoa kauli yenye kudai kuwa anao mkanda
wa video unaoonesha namna tukio lilivyotendeka na akasisitiza kuwa
mlipuaji ni askari polisi aliyekuwa amevalia sare za kikosi cha kutuliza
ghasia (FFU).
Upande mwingine, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alirusha kombora kwamba Chadema ndiyo
wahusika wa bomu hilo.
Tuhuma za Nape, zinaendana na dhana kuwa
Chadema walijilipua wenyewe kwa lengo la kutafuta huruma ya wapiga kura
ili wakichague chenyewe katika uchaguzi mdogo wa udiwani, uliofanyika
Juni 16, mwaka huu.
Uchunguzi unapingana na dhana hiyo kwa hoja
kwamba Chadema kilikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika
uchaguzi huo bila hata kusaka huruma ya wapiga kura, kutokana na jinsi
kilivyokuwa kinakubalika.
Macho yanayoona mbali aliyonayo Naibu
Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ndiyo yaliyomuongoza
pale alipowataka wanasiasa kukaa kimya na kuacha mamlaka zinazohusika
kufanya kazi yake.
“Natoa rambirambi zangu na kulaani. Naamini katika
mambo haya ni vyema wanasiasa tukafunga midomo yetu hadi ukweli
ujulikane,” January, aliandika ujumbe huo kuhusiana na tukio la Arusha,
kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.
Wakati January akiwataka watu
kutulia na kuacha kusemasema, Noel Kyaro ambaye ni mwongozaji wa watalii
(tour guider) Arusha, alisema kuwa kama Chadema na CCM, watakaa pamoja
na kuacha kutuhumiana, wanaweza kumpata kwa urahisi mhusika wa mabomu.
“Kuna
changamoto nzito hapa, inabidi pia tuangalie uhusiano wa nchi yetu na
mataifa mengine. Tanzania inaonewa wivu sana kutokana na uimara wake wa
vivutio vya utalii,” alisema Kyaro na kuongeza:
“Hivi karibuni Rais
wa Rwanda, Paul Kagame, alitoa kauli chafu sana dhidi ya Rais Jakaya
Kikwete. Sasa haishindikani Rwanda kufanya huo ugaidi kwa sababu
wameonesha waziwazi kupitia kwa rais wao kuwa hawatupendi.”
Rwanda
inapotajwa, moja kwa moja kikundi cha waasi cha chini DRC cha M23,
kinaingizwa katika skendo hiyo kwa sababu haijapita muda mrefu tangu
nacho kiutangazie ulimwengu kuwa kitapambana na Tanzania.
Mei 5,
mwaka huu (Jumapili), saa 4:30 asubuhi, bomu lilirushwa kwenye Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Arusha na
kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi zaidi ya 40.
Siku moja
kabla, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, alitoa tamko la serikali kuwa Tanzania lazima ipeleke majeshi DRC
kupigania amani na haitishwi na vitisho vya waasi wa M23.
Kauli ya
Membe, ilifuatia waraka wa M23 ambao waliutuma nchini, wakieleza kuwa ni
ujumbe kutoka kwa Mungu, wakiionya Tanzania kutopeleka majeshi DRC,
vinginevyo itakiona cha moto.
Baada ya kauli hiyo ya Membe, M23 walihamishia mashambulizi yao kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, wakiitishia Tanzania.
Baadhi
ya ‘twiti’ za M23, siku moja kabla ya bomu la kanisani Arusha, mojawapo
ilisema: “Membe usiwadanganye watu, mnakuja DRC kuweka petroli kwenye
moto, hamji kutafuta amani.”
Twiti nyingine inasomeka: “Hatutishwi na scout (askari chipukizi), Tanzania leteni majeshi yenu halafu mtaona.”
Hatari
kubwa zaidi ni kwamba M23, walitishia kuingia nchini na kufanya
mashambulizi, wakitamba wana uwezo mkubwa sana wa kufanya hivyo.
Kutokana
na hatari hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe,
‘alitwiti’, akionya kwamba M23 walikuwa ‘wanatwiti’ wakiwa Dar es
Salaam, hivyo ni dhahiri kuwa kundi hilo lilikuwa limeshaingia nchini.
Kauli
hiyo ya Zitto, ilikuwa inaweka wazi namna taifa letu lilivyo hatarini,
kwani maadui wanaweza kuingia nchini na kupanga mashambulizi dhidi yetu
bila sisi wenyewe kujua.
“Kabla ya kurushiana makombora na
kutuhumiana bila ushahidi ni bora tukaangalia uhusiano wa nchi yetu na
mataifa mengine. Nchi majirani zetu hazitupendi, wanatuonea wivu,
hawashindwi kupanga njama za kutuchonganisha sisi kwa sisi,” alisema
Matilda Urio wa Kijenge Chini, Arusha na kuongeza:
“Hatutamjua adui,
hatutapata ufumbuzi wa haya matatizo mpaka tutakapoacha kutuhumiana sisi
kwa sisi. Chadema waache kuwalaumu CCM kuwa wanahusika, vilevile CCM
wasiituhumu Chadema. Tuhuma hizo zinapoteza uelekeo wa kumjua adui.”
Mtumiaji
wa Twitter mwenye akaunti yenye jina @iAlen, aliandika ujumbe wake kwa
Lugha ya Kiingereza; This Chadema CCM blame game isn’t going to help
anyone. People have lost their lives here folks (Huu mchezo wa
kulaumiana CCM na Chadema hautamsaidia yeyote. Watu wamepoteza maisha).
KWA NINI
NI WATU WA NJE?
Kwa
mujibu wa watu waliozungumza na gazeti hili ambao wanalitazama tukio la
Arusha kwa jicho la mbali zaidi ni kwamba sura ya nchi kiutalii ndiyo
inayosababisha jiji hilo likumbwe na misukosuko ya milipuko ya mabomu.
“Unalengwa
utalii wetu, majirani wanataka Tanzania ionekane ina machafuko ili
watalii wawe wanaenda kwenye nchi zao,” alisema Rachel Komba ambaye ni
Meneja Uhusiano wa Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya OTSG.
Rachel
alisema: “Jinsi tunavyogombana ni sawa na mgonjwa wa kifafa halafu
arogwe ugonjwa wa malaria ya kichwa, akianguka, kila mtu atajua kifafa
ndicho kimemfanya aanguke.
“Tanzania kuna udini, kuna mvutano mkubwa
wa kisiasa kati ya CCM na Chadema. Bomu likitupwa kanisani, haraka sana
Wakristo wanawatuhumu Waislamu, vilevile bomu likitupwa kwenye mkutano
wa Chadema, wafuasi wa Chadema watawatuhumu CCM.
“Tuliona jinsi bomu
la kanisani Arusha lilivyoleta sintofahamu, vilevile hili la mkutano wa
Chadema, linavyowagombanisha CCM na Chadema. Kuna adui wa nje
anayewachonganisha Watanzania.
“Anafanya makusudi kwa kutumia udhaifu
wetu. Anajua tuna udini, anapiga upande mmoja halafu Waislamu na
Wakristo wanakamatana, amepiga mkutano wa Chadema, tunaona hali ilivyo.”
Rachel
aliongeza: “Inakuwa vigumu kuwajua hawa maadui kwa sababu wanatupiga
kwa kutuchonganisha. Kama wangelipua reli au bandari, moja kwa moja
tungejua ni wavamizi kutoka nje. Tatizo wanapiga makanisa, misikiti na
mikutano ya vyama vya siasa ndiyo maana inatuchukua wepesi kutuhumiana
sisi kwa sisi.”
Elibariki Munishi wa Unga Limited, Arusha,
alikumbusha tukio la bomu ambalo alipigwa Katibu wa Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha, Sheikh Abdulkarim Jonjo,
akiwa nyumbani kwake na kumjeruhi vibaya.
“Inawezekana kabisa, watu
waliomrushia bomu Sheikh Abdulkarim ndiyo haohao waliolishambulia kanisa
na ni haohao waliorusha kwenye mkutano wa Chadema. Inabidi tuwe makini
sana.
“Tukidanganyika, tunaweza kupigana sisi kwa sisi. Hakuna
Muislamu Mtanzania anayeweza kumdhuru Mkristo, vilevile Mkristo hawezi
kumdhuru Muislamu kutokana na asili yetu na tunavyojijua,” Elibariki.
LENGO LA NINI?
John Sebless wa Ngarenaro, alisema kuwa lengo la adui ni kuvuruga sura ya utalii wa nchi, hivyo kuyafaidisha mataifa ya kigeni.
“Haya
machafuko malengo ya wachafuaji ni kuifanya nchi yetu ionekane siyo
salama kwa kupokea watalii. Halafu jiulize kwa nini Arusha ambayo ndiyo
mji ambao unaoongoza kwa utalii nchini?
“Tunatakiwa kuacha kulumbana
na kusimamia utaifa wetu. Adui kutoka nje anatugawa, tuache kuzingatia
mambo ya msingi na matokeo yake tubaki tunalumbana wenyewe. CCM hakiwezi
kulipua bomu Chadema kwa sababu viongozi wake wana akili na wanajua
kufanya hivyo, wao watakuwa watuhumiwa nambari moja.
“Vilevile
haiingii akilini Chadema kujilipua wenyewe. Tuache kulumbana, Wakristo
kwa Waislamu, Chadema, CCM na vyama vingine vyote, tunatakiwa tutambue
kwamba tumevamiwa kisha tuanze kupambana na adui huyo wa nje anayetaka
kuvuruga sifa njema ya nchi yetu kiutalii,” alisema Sebless.
Hata
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, mapema wiki hii,
alithubutu kulinyooshea kidole jeshi la polisi, akalitaka kuacha kutumia
mabomu kutuliza machafuko, akafafanua kwamba kufanya hivyo kunazidi
kuuweka utalii wa nchi katika hali mbaya.
KUTOKA KWA MHARIRI
Tunapaswa
kulinda amani yetu ambayo inavutia watalii na wawekezaji wengi kuja
nchini. Tuamke sasa na kupambana na adui anayetaka kuivuruga nchi yetu.
Bila umoja na mshikamano hatutashinda. Tusikubali kuchochewa kupigana
sisi kwa sisi. MHARIRI.