Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), imepanga kuanza kuwadahili wanafunzi wa
 kujiunga na masomo ya vyuo vikuu kwa kutumia uzoefu wao.
Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha
 wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini 
walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.
Kupitia utaratibu huo mpya, mtahiniwa atajiunga na Chuo Kikuu kulingana 
na fani atakayoiomba na atatakiwa kufanya mitihani mitatu na kufaulu kwa
 wastani wa daraja B.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu kutoka TCU, Dk Savinus 
Maronga aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona kuna watu wengi 
wanaopenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu, lakini wameshindwa 
kutokana na kutokuwa na vigezo, TCU imeamua kuanzisha mitihani hiyo 
maalumu.
Alisema kuwa mfumo huo unaojulikana kama ‘Recognition of Prior Learning’
 (RPL), utamwezesha mwombaji kudahiliwa vyuoni kupitia tume hiyo kama 
wanavyofanya watahiniwa wengine.
Sifa zinazotakiwa
Kuhusu sifa za kujiunga, Dk Maronga alisema kuwa mwombaji anatakiwa kuwa
 na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea, sambamba na kuwa na elimu 
isiyopungua darasa la saba.
“Mwombaji anatakiwa kuwa na nia ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu na uzoefu wa kile ambacho anakusudia kukisoma.
Awe na uwezo wa kuandika na kusoma Lugha ya Kiingereza, ambayo ndiyo 
inayotumika kufundishia vyuoni,”alisema Dk Maronga na kuongeza:
“Kuna watu wameishia darasa la saba, lakini wamefanya kazi katika eneo 
moja, mfano karani wa mahakama, mwandishi wa habari kwa muda mrefu. 
Hivyo mfumo huu utawawezesha kuendelea na masomo bila tatizo.”
Vigezo
Mkurugenzi huyo alisema, kutakuwa na mitihani ya masomo matatu, ambayo 
mtahiniwa ili apate nafasi ya kuendelea na masomo ni lazima afaulu kwa 
wastani wa daraja B.
Alisema daraja la kwanza linaloanza na alama A ni 75-100, daraja B+ ni 
60-75, B ni 50-59, C ni 40-49, D ni 35-39 na daraja E ni 0-34.
“Katika mitihani mitatu atakayoifanya, atatakiwa kupata wastani wa 
daraja ‘B’ na somo husika la fani yake atatakiwa kupata alama B ili kuwa
 na vigezo vya kupata cheti kitakachomwezesha kuendelea na masomo 
yake,”alisema Dk Maronga.
chanzo:gazeti la mwananchi