| 
| 'Hekalu' linalomilikiwa na Mchungaji Getrude Lwakatare. | 
  | 
  | 
Wabunge
 wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Terezya 
Huvisa kuzivunja nyumba mbili zilizopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam 
zilizojengwa katika fukwe ya bahari ya Hindi ikiwemo ya mbunge licha ya 
kwamba kuna zuio la mahakama.
Bila
 kutaja majina ya wamiliki hao, wabunge hao walitaka hatua hizo 
zichukuliwe kwa haraka kwa nyumba hizo zilizojengwa kwenye fukwe kinyume
 cha sheria zivunjwe kwa maelezo kuwa hazina ofa wala hati. 
  
Sambamba
 na hilo wametaka watendaji wa serikali waliohusika kutoa vibali 
kuruhusu ujenzi huo kwa maelezo kuwa walichukua rushwa wachukuliwe 
hatua.
 
 Mbunge wa kwanza kuanza kuzungumzia hilo ni wa viti maalum, 
Esther Bulaya (CCM) aliyetaja viwanja viwili vyenye namba 2019 na 2020 
kikiwemo cha mbunge ambaye ni kiongozi wa kiimani waliojenga  nyumba 
zivunjwe licha ya kuwepo zuio la mahakama.
 
 “Mwaka jana waziri wa 
Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka alivunja nyumba za kawaida licha ya zuio 
la mahakama, lakini nyumba zilizo kwenye viwanja namba 2019 na 2020 
hazikuvunjwa kwa sababu ya zuio la mahakama hii ni double standard 
hatuwezi kuvumilia. 
“Wengine wenye nyumba ni viongozi tupo nao humu 
tena wa kiimani, lakini kwa nini viongozi tunafaya hivi wakati 
tunatakiwa tuwe wa mfano na tunawafanya viongozi wenzetu washindwe 
kufanya kazi zao?…hakuna haja ya kuogopa waziri Huvisa (Mazingira) vunja
 nyumba, haiwezekani kuwa na nguvu ya fedha.
 
 “Wabunge wenzangu 
tuazimie Manispaa ya Kinondoni na NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na 
Usimamizi wa Mazingira), wakavunje nyumba hizo ndani ya wiki moja , 
naomba kutoa hoja,” alisema.
 
 Hata hivyo, Spika Anne Makinda alimweleza; “Haiwezekani kutoa hoja kwa kuingilia vyombo vingine”.
 
 Mbunge
 ambaye ni kiongozi wa kiimani mwenye nyumba katika  eneo hilo la Mbezi 
Beach aliyejenga katika fukwe ya bahari kwa kuondoa mikoko na kuweka 
kifusi na kujenga nyumba ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Dk. 
Getrude Lwakatare (CCM).
Naye Mbunge wa viti maalumu, Grace Kiwelu 
(Chadema) akichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, alisema kamati 
yake ya Ardhi na Mazingira ilitembelea eneo hilo la Mbezi Beach na 
kukuta aliyejenga katika kiwanja 2019 hakuwa na ofa wala hati.
 
 “Ametumia
 pesa kuwarubuni watendaji akaondoa mikoko, akaweka kifusi na akajenga 
nyumba naomba wizara ya Ardhi na ya mazingira wawachukulie hatua 
watendaiji hao,” alisema. 
Akijibu hoja ya Bulaya, kuwa kwanini 
nyumba ya Mchungaji Lwakatare haikuvunjwa wakati nyingine zilivunjwa, 
mwanasheria mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema: 
  
“Sisi ni wajibu 
wetu twende mahakamani kusema watu hao wamevunja sheria kujenga hapo. 
Wao wanaruhusiwa na Katiba na mahakama itafuata sheria.
“Nashauri Bulaya usitoe shilingi kuzuia Bajeti ya Waziri, uje tuone huyo kigogo itakuwaje.” 
Hata hivyo, Huvisa alisema: “Nyumba tulizovunja hazikuwa na kesi na hii tuliyoiacha ilikuwa na kesi.”
Jumba
 la kifahari linalodaiwa kuwa la Mchungaji Lwakatare ambalo 
lilizinduliwa mwaka jana, limekuwa klikitajwa kuwa lina thamani ya 
takribani sh bilioni 1.5.
zero99