Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya Watanzania katika maadhimisho ya miaka 49 ya muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na baadaye kusamehe wafungwa 4,180.
Idadi kubwa ya watanzania walishiriki katika maadhimisho hayo
hayo ambayo yalianza saa 2:30 asubuhi na kupambwa na gwaride rasmi
lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na
kupendezeshwa na halaiki ya wanafunzi 2,695 kutoka Tanzania Bara na
Visiwani waliofanya maonyesho mbalimbali ya kuashiria maadhimisho ya
muungano.
Viongozi mbalimbali wakiwamo wastaafu kutoka Tanzania Bara na
Visiwani walishiriki kwenye maadhimisho hayo ikiwa ni ishara ya kuuenzi
na kuulinda muungano huo.
Viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu
wa Rais wa Tanzania, Dk Mohamed Gharib Bilali, Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad na
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd.
Wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Rais mstaafu wa Zanzibar,
Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi,
Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick
Sumaye.
Baada ya viongozi kuketi katika nafasi zao, gwaride rasmi lenye gadi
kumi lilipita na kutoa heshima zao mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Baada ya hapo vijana wa halaiki walionyesha maumbo mbalimbali
kuashiria maendeleo yaliyopatikana nchini kwa muda wa miaka 49 tokea
taifa la Tanzania liundwe rasmi kabla ya Wanahalaiki kujipanga na
kuonyesha taswira mbalimbali na kuimba wimbo wa kuhamasisha kudumisha
muungano.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani hawakuweza kushiriki kwenye maonyesho hayo.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa shughuli za maadhimisho hayo, mjumbe wa Kamati Kuu Chadema ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema kuwa, Watanzania wanapaswa kujivunia Muungano walionao kwa sababu umedumu kwa miaka 49, akieleza kuwa ni nadra sana kuona nchi za Afrika au Ulaya kuendeleza muungano wenye umri mkubwa kama huu wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo basi wanapaswa kuuenzi na kuulinda kuendeleza amani iliyopo.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,180
waliokuwa wakitumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali hapa
nchini katika kuadhimisha miaka 49 ya muungano.
Wafungwa waliosamehewa ni wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka
mitano, ambapo mpaka siku ya msamaha yaani April 26, watakuwa
wameshatumikia robo ya vifungo vyao, wafungwa wagonjwa wa Ukimwi, kifua
kikuu na kansa ambao wamethibitishwa na jopo la madaktari.
Pia wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike
walioingia na mimba gerezani, walioingia na watoto wanaonyonya na
wasionyonya, wakiwamo walemavu.
Msamaha wa Rais pia umeenda kwa wafungwa walemavu wa mwili na akili
na wafungwa ambao hadi siku ya jana walikuwa wameshakaa gerezani kwa
muda wa miaka mitano na wameonyesha kuwa na tabia nzuri.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Chanzo: mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment