Wednesday, March 20, 2013

MJADALA: ZIDANE, INIESTA NANI ZAIDI?

MJADALA: ZIDANE, INIESTA NANI ZAIDI?


ZINEDINE Zidane ni mmoja wa wachezaji wenye kipaji cha aina yake waliowahi kucheza soka akiwa na Ronaldo De Lima.

Akiwa na umri mdogo, Zidane alikuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza mashambulizi kupitia katikati ya uwanja huku akitumia uwezo binafsi na nguvu ipasavyo.

Wakati huo alikuwa akichezea klabu ya Bordeux ya Ufaransa kabla hajasajiliwa na Juventus ya Italia kwa ada ya uhamisho ya thamani ya pauni milioni tatu ambazo ni zaidi ya Sh. 7.5 Bilioni.

Akiwa na Juventus, Zidane hakuanza maisha vyema na kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa na walakini na uwezo wake.

Kadri msimu wa mwaka 1996/97 ulivyozidi kwenda, Zidane taratibu alianza kuonekana muhimu na alikuwa na mchango mkubwa kwa kikosi kilichofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambacho kwa bahati mbaya kilifungwa na Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Kipigo hicho kilipokewa kwa mshangao na wengi hasa baada ya Zidane maarufu kama Zizzou kukabwa ‘man to man’ kwenye mchezo huo na kiungo wa Dortmund, Paul Lambert ambaye hii leo ni kocha wa Aston Villa.

                
Msimu uliofuata, Juventus ilifungwa katika fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid kwa bao la Predrag Mijatovic. Kikosi hiki cha Juventus kilichokuwa na Didier Deschamps, Edgar Davids, Alesandro Del Piero na Zizzou kilikuwa kinaonekana kama kitatawala soka la Ulaya kwa muda mrefu ujao.


Kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998, Zidane alilazimika kungoja hadi mchezo wa fainali kisha kufunga mabao yake ya kwanza ya michuano hiyo. Mabao hayo ndiyo yaliyoipa Ufaransa ubingwa wa Dunia kwa mara ya kwanza, na hapa hakukuwa na ubishi kuwa, Zidane alikuwa mchezaji bora mbele ya kizazi cha dhahabu cha wachezaji wa Les Bleus.


Miaka miwili baadaye, Ufaransa ilitwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Ulaya licha ya Zidane kutofunga bao hata moja. Hakuna ubishi kuhusu mchango alioutoa katika mafanikio hayo ya Ufaransa mwaka 2000.



MCHEZAJI GHALI KULIKO WOTE DUNIANI

 

Mwaka 2001 Zidane aliuzwa kwenda klabu ya Real Madrid kwa dau lililoweka rekodi ya Dunia kwa wakati huo la pauni milioni 42 ambazo ni zaidi ya Sh. 105 Bilioni.

Msimu wake wa kwanza akiwa na Real Madrid, ulikuwa mgumu na kulikuwa na taarifa kuwa, presha ya matarajio makubwa yaliyokuwepo mabegani mwake kutokana na fedha nyingi zilizotumika kumsajili ilikuwa kubwa kwake.

Hata hivyo, Real Madrid ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2002 na kwenye fainali yake ya tatu, Zidane alifanikiwa kutimiza ndoto zake.


Kwenye fainali hiyo, Zidane alifunga bao ambalo linaweza kuwa bora kwa miaka yote ya michuano hiyo.

Zidane alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa Dunia mwaka 2003, ikiwa mara yake ya tatu kupewa tuzo hiyo. Kabla ya hapo aliwahi kutwaa tuzo hiyo kwenye miaka ya 1998 na 2000.


Uwezo wake wa kubadili matokeo ya mechi ngumu uwanjani, ulimfanya adhihirishe ubora wake mbele ya kila mtu. Kwenye klabu yake, kulikuwa na ‘issue’ za mradi wa Galactico ambazo ziliathiri mafanikio ya klabu.

Ulikuwa wakati mgumu kwa Zidane kwa kuwa hata timu yake ya taifa ilikuwa na matatizo kwenye michuano mikubwa. Majeraha aliyopata mwaka 2002 yalishuhudia timu yake ikitemeshwa ubingwa wa Dunia kwenye hatua ya makundi.Ufaransa ilishindwa kupata hata bao moja.

Timu zote mbili za Zidane, kwa maana ya Ufaransa na Real Madrid zilikosa ‘balance’ na hii ilimnyima mafanikio japo aliyopata kwenye tuzo binafsi mojawapo ikiwa ya kuteuliwa kuwa mmoja wa wachezaji 50 bora wa miaka yote.



Mwaka 2006 ulikuwa wa aina yake kwenye historia ya mchezo wa soka. Mwaka 2003 Barcelona walimnunua Ronaldinho Gaucho wakati Real Madrid walimnunua David Beckham. Wachezaji hawa wawili walikuwa gumzo na walionyesha mwelekeo wa mchezo wa soka kwa kipindi hicho.


Beckham alionekana kuwa mtu aliyejengwa kwenye miaka ya 90 na Gaucho akionekana wa miaka ijayo. Wakati Madrid na mradi wao wa Galactico wakionekana ‘wana-flop’, Barcelona walikuwa wakicheza soka safi na la kuvutia.

Mwaka 2006 walitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiifunga Arsenal mabao 2-1. Mtindo wao wa soka lao la kushambulia kwa pasi nyingi huku ukiongozwa na Samuel Eto’o na Gaucho, ulivutia machoni kwa watazamaji. Haya yalikuwa mapinduzi ya soka.

Mwaka huo pia kulikuwa na Kombe la Dunia huko Ujerumani. Zidane aliamua kurejea kwenye timu ya taifa na kuiongoza Ufaransa kwa mara ya mwisho. Mkataba wake na Real Madrid uliisha msimu wa 2005/06 na katika michuano ya Kombe la Dunia 2006, ndipo alipocheza soka kwa mara ya mwisho.


MCHEZO ULIOLETA MABADILIKO.


Kama ndoto, Zidane aliiifikisha Ufaransa hadi fainali ya Kombe la Dunia 2006. Mechi ambayo itakumbukwa na wengi ilikuwa robo fainali dhidi ya Brazil, ambapo ilikuwa vita yake na Ronaldinho Gaucho.

Ilikuwa inaonekana kama imepangwa kwa Ufaransa na Zidane kutwaa ubingwa wa Dunia na kwenye fainali alifunga bao la mkwaju wa penati ambalo lilimfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanne pekee ambao wamewahi kufunga kwenye fainali mbili tofauti.


Hata mchezo huo ulipomalizika katika muda wa kawaida, ulilazimika kuamuliwa kwa muda wa nyongeza ambako Zidane almanusra afunge bao kwa kichwa lakini mpira aliopiga uligonga mwamba. 


Kwa mshangao wa wengi, Zidane alionyeshwa kadi nyekundu zikiwa zimebaki dakika kumi fainali ifikie hatua ya matuta baada ya kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi.

Ufaransa iliishia kufungwa kwa mikwaju ya penalti na wengi walifikiri kuwa endapo Zidane asingetolewa, Ufaransa ingekuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wao wa pili.

Fainali hiyo ilikuwa siku ambayo mabadiliko yalifanyika ambapo ‘master’ wa soka kwa muongo uliopita yaani Zidane, alikuwa anamaliza zama zake na kijana ambaye anakuja kurithi nafasi yake alikuwa anaanza taratibu.


KIUNGO MCHEZESHAJI BORA


Mwaka 2006 kundi la watu liliamua kuanzisha tuzo maalum kwa viungo wachezeshaji, tuzo ambayo ilipewa jina la WORLD PLAYMAKER AWARD yaani kiungo mchezeshaji bora, na tuzo ya kwanza kwa mwaka huo ilikwenda kwa Zidane.

Ilikuwa njia nzuri ya kumuenzi kiungo mchezeshaji bora wa kizazi cha hivi karibuni. Kaka alishinda mwaka uliofuatia na kwa upande wake alikuwa kama Zidane kwa njia nyingi.

Mwaka 2008, kiungo mchezeshaji wa aina mpya aliibuka. Aliwahi kuwepo tangu awali, ila kwa mwaka huo alianza kuchukua nafasi yake kama mtu muhimu kwenye timu alizochezea, alianza kutawala mechi alizocheza katika njia ambayo ilisababisha ushindi kwa timu yake.


Mashabiki walianza kuona kile ambacho anafanya akiwa uwanjani, jinsi alivyokuwa akiwaongoza wenzake uwanjani. Xavi Hernandez ndiye kiungo mchezeshaji anayezungumziwa.

Mwaka 2006 pia ulikuwa mwaka ambao Barcelona walianza kutambulika kama timu ya kuogopwa Ulaya, na mwaka 2008 timu ya taifa ya Hispania kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya, ilianza rasmi safari yake kuelekea mafanikio ya kiwango cha juu.

Mchezo wa soka ambao ulikuwa ukitegemea zaidi nguvu katika miaka iliyopita ulianza kubadilika. Barcelona na Hispania zikiwa na wachezaji wadogo kimaumbo lakini wenye uwezo mkubwa kimbinu na kiuwezo kama Xavi Hernandez, Andres Iniesta na Lionel Messi zilibadilisha jinsi soka la Ulaya lilivyochezwa na wachezaji hawa wakiibuka kama wachezeshaji wapya kwenye soka.

Xavi Hernandez alishinda tuzo ya kiungo mchezeshaji bora kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2008 mpaka 2011. Alistahili tuzo hiyo na alistahili tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 2008.


Xavi aliziongoza Barcelona na Hispania kupata mafanikio kwa miaka minne akitwaa mataji karibu yote kwenye soka la klabu na timu ya taifa. Xavi alikuwa kama funguo iliyofanya wenzie wacheze vizuri.
     

 
Mwaka 2012, tuzo ya kiungo mchezeshaji bora ilihamia kwa mwenzie Andres Iniesta. Michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya 2012 ilimshuhudia Xavi akitwaa tuzo ya mchezaji bora na alimaliza kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Cristiano Ronaldo na Messi kwenye tuzo za Ballon D’or.

Hatimaye Iniesta alitambuliwa kama mmoja wa wachezaji bora. Miaka kumi ikiwa imepita tangu Zidane alipotwaa ubingwa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Real Madrid pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa dunia, kiungo mchezeshaji wa aina mpya alichukua mikoba ya Zidane akiwa anacheza kwa staili tofauti na Zidane lakini kwa ubora, kiwango na matokeo yale yale .



KIUNGO MCHEZESHAJI ALIYEKAMILIKA


Andres Iniesta alianzia soka lake akiwa kwenye Academy ya La Massia inayomilikiwa na Barcelona. Uwezo wake wa kucheza kwenye nafasi tofauti, kujituma, na umuhimu kwenye mchezo, ulimfanya achukua nafasi kwenye kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 18 na alianza kucheza mechi mfululizo kwenye msimu wa mwaka 2004/05.

Akiwa kama mchezaji mchanga, Iniesta alianza kufanya mazoezi akiwa na kikosi cha kwanza na Pep Guardiola (kocha wa zamani wa Barcelona wakati akiwa bado mchezaji) alimwambia Xavi kuwa, yeye (Xavi) angemfanya Guardiola astaafu lakini Iniesta atawafanya wote wawili yaani Xavi na Pep wastaafu.


Pep Guardiola na Andres Iniesta

Guardiola aliona mbali na hakukosea kwa kauli aliyoitoa, Iniesta hakuwa bora kwenye pasi pekee bali alikuwa mzuri kwenye ukokotaji wa mpira, alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza maeneo tofauti ya uwanja na alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kutoa pasi muhimu.


Ilikuwa chini ya Guardiola ambapo Iniesta aliuteka ulimwengu. Guardiola alimtengeneza Iniesta na kumfanya kuwa mchezaji muhimu kwa Barcelona na Hispania na kubwa alilofanya Guardiola ni kumfanya Iniesta ambaye kwa kawaida ni mtu mkimya, kuwa kiongozi kwenye timu yake.


Chini ya nahodha huyu wa zamani wa Barcelona, soka la Iniesta lilifikia kiwango cha juu kupita hata Xavi na Guardiola kama ilivyokuwa kauli ya Guardiola. Alikuwa kiungo mchezeshaji aliyekamilika na hadi sasa ameingia kwenye orodha ya wachezaji bora waliowahi kucheza Barcelona.


MFUNGAJI WA MABAO MUHIMU

Iniesta siyo mfungaji wa mabao mengi, lakini ni mfungaji wa mabao mazuri na muhimu kwa timu yake kama Zidane. Iniesta alikuwa akifunga kwenye mechi muhimu na kubwa.

Moja ya mabao ambayo yatakumbukwa na wengi ni bao alilowafunga Chelsea mwaka 2009 kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ulikuwa mpira wa mwisho kwenye mechi hiyo na ulikuwa mpira ambao Iniesta alifunga bao lililoivusha Barcelona hadi fainali.


Kwenye Kombe la Dunia 2010, Iniesta alifunga bao muhimu kwenye historia ya soka la Hispania. Huku ubao wa matokeo ukisomeka 0-0 wakati wa fainali hiyo dhidi ya Uholanzi, mpira ulimfikia Iniesta upande wa kulia wa eneo la 18, halikuwa bao kama la Zidane kwenye fainali ya mwaka 2002 wakati Real Madrid walipocheza na Bayer Leverkusen, lakini umuhimu wake ulikuwa ule ule.

Zidane alitwaa Kombe la Dunia na ubingwa wa Ulaya akiwa na Ufaransa, lakini hakuweza kutwaa mataji matatu mfululizo na hakuna yeyote aliyewahi kufanya hivyo kabla.


Hispania waliweka historia hiyo na Iniesta alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya 2012. Aliiongoza timu yake akiwa ndani ya uwanja kwa uwezo wake na miaka minne baada ya Xavi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya 2008, Iniesta alitimiza utabiri wa Guardiola.


 

Kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2011, Kocha wa Manchester United, Sir. Alex Ferguson alisema kuwa, kwake Messi si mchezaji anayemuogopa, anamuogopa zaidi Iniesta kwani ndiye hasa mwenye funguo za Barcelona kwa jinsi anavyotafuta upenyo wa kupitisha mipira kwa wenzake na mabao yake muhimu.


Vicente Del Bosque ambaye aliwahi kufanya kazi na Zidane kwenye klabu ya Real Madrid, alimtaja Iniesta kama mchezaji aliyekamilika kuliko wote aliowahi kuwaona.

Na mchezaji mwingine, Samuel Eto’o alimtaja Iniesta kama mchezaji bora duniani kwani kila awapo uwanjani huwa anatengeneza maajabu.

Hakuna ubishi kuwa Iniesta amekuwa akibadilika kwenye nafasi ya kiungo mchezeshaji bora kuendana na mchezo wa soka kwa zama za sasa.

Akiwa kwenye mfumo wa Barcelona huku akicheza soka kuendana na umbo lake dogo, Iniesta alijifunza kumiliki mpira na kuuelewa mchezo kwa jinsi anavyotengeneza ‘movement’ zake, mbinu na hata maamuzi ambayo anayafanya, kitu kinachofanya soka kuonekana rahisi kwake. 

0 comments: