Na Fadhy Mtanga
REAL
Madrid imejihakikishia kucheza robo fainali ya michuano ya Ligi ya
Mabingwa barani Ulaya baada ya kuitandika Schalke 04 ya Ujerumani mabao
6-1. Mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo, mchezaji aliyevunja
rekodi ya usajili ulimwenguni Gareth Bale pamoja na mchezaji mahiri
Karim Benzema walihakikisha kila mmoja wao anatupia nyavuni magoli
mawili ili kuifanya Real Madrid, vinara wa ligi kuu nchini Hispania,
kuisulubu vilivyo Schalke 04 tena kwenda dimba lake la nyumbani,
Veltins-Arena. Bao la kufutia machozi la Wajerumani hao lilifungwa na
Klaas Jan Huntelaar katika dakika ya 90.
Alikuwa
Karim Benzema katika dakika ya 13 tu alipopokea mpira kutoka kwa
Cristiano Ronaldo na kuutumbukiza wavuni kama ishara ya ufunguzi rasmi
wa karamu ya magoli ya miamba hao wa soka nchini Hispania. Kisha, panapo
dakika ya 21, mchezaji aghali zaidi aliyesajiliwa kutoka Tottenham
Hotspur ya Uingereza, Gareth Bale akautia mpira kimiani baada ya kupokea
pasi kutoka kwa Karim Benzema.
Mwamuzi
Howard Webb, anayetajwa kuwa mwamuzi bora zaidi duniani kwa sasa
alipopuliza kipenga kuashiria mapumziko, Real Madrid wakarejea vyumba
vya mapumziko wakiwa tayari na magoli mawili nunge.
Timu hizo
ziliporejea dimbani kwa ngwe ya mwisho, ilimchukua Cristiano Ronaldo
dakika saba tu kuibadili pasi kutoka kwa Gareth Bale kuwa goli la tatu.
Dakika tano baadaye, dakika ya 57, Karim Benzem akafungua awali ya pili
ya ufungaji kwa wasukuma ndinga hao machachari alipofunga bao la nne
dhidi ya Schalke 04. Kama ilivyo kanuni ya hesabu za pythagoras, Karim
alifunga goli hilo kwa kupata usaidizi kutoka kwa yule yule aliyempa
pasi awali, Cristiano Ronaldo.
Dakika ya
69 ya mchezo, ikawa zamu tena ya Gareth Bale kuutia mpira wavuni baada
ya kupokea pasi nzuri ya Sergio Ramos. Ubao wa matokeo ukasoma Schalke
04 0 Real Madrid 5. Matokeo hayo yalidumu kwa dakika 20 tu kwani panapo
dakika ya 89 ya mchezo krosi ya Karim Benzema ikamfikia Cristiano
Ronaldo. Naye hakufanya ajizi, akaitia wavuni na kuwafanya mashabiki wa
Real Madrid kote ulimwenungi kushangilia kwa tambo na kujidai kwa kila
namna.
Dakika
iliyofuata, Klaas Jan Huntelaar aliyekuwa tayari amelimwa kadi ya njano
panapo dakika ya 72, akafunga bao la kuwafutia machozi wenyeji wa mchezo
huo.
Kwa
matokeo hayo, Schalke 04 inahitaji miujiza ili isonge mbele. Timu hizo
zinatarajia kukwaana tena katika mchezo wa pili utakaokimbizwa dimbani
Santiago Bernabeu jijini Madrid, Hispania majuma matatu yajayo.
Kwingine
barani Ulaya, Galatasaray iliikaribisha Chelsea, vinara wa ligi kuu ya
Uingereza. Dakika ya 9 tu ya mchezo huo uliopigwa katika dimba la Turk
Telekom, Fernando Torres akaifungia Chelsea goli la kuongoza. Chelsea
ikawa timu ya kwanza kutoka Uingereza kufunga goli katika hatua hiyo ya
16 ya michuano ya UEFA. Timu zingine kutoka Uingereza, Machester City,
Arsenal na Manchester United ziliambulia kichapo cha magoli 2-0 kutoka
kwa Barcelona, Bayern Munich na Olympiakos.
Chelsea
iliendelea kuongoza ikiwa ugenini hadi dakika ya 65 pale Aurelien
Chedjou alipofunga akisaidiwa na Wesley Sneijer. Matokeo hayo yanaipa
ahueni ya goli la ugenini Chelsea. Timu hizo zinatarajia kutimuliana
vumbi tena wiki tatu zijazo pale mitaa ya Fulham, London katika dimba la
Stamford Bridge.
0 comments:
Post a Comment