Mkutano
wa 11 unaendeleo leo mjini Dodoma, ambapo Bajeti ya Wizara ya Maji
iliyokwama kupitishwa baada ya wabunge kuigomea, inatarajiwa
kuwasilishwa, ikiwa na maboresho, hususani eneo la nyongeza ya fedha
katika miradi ya maji.
Bajeti hiyo ilitarajiwa kupitishwa tangu Alhamisi wiki iliyopita, lakini kutokana na ufinyu wa fedha zilizotengwa, takribani wabunge wote waliochangia mjadala wake, wakiwemo wa CCM, waligoma kuiunga mkono.
Kutokana
na hali hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema suala la maji
haliwezi kufanyiwa utani na kuitaka Wizara ya Maji, Kamati ya Bajeti na
Wizara ya Fedha, kufanyia kazi suala hilo na walete majibu ya uhakika.
Leo
wabunge hao wanatarajia upande wa Serikali kuwasilisha bajeti hiyo,
ikiwa na maboresho mapya ya nyongeza ya fedha za miradi inayotarajiwa
kufikia zaidi ya Sh milioni 185, ambazo wabunge hao walipendekeza ili
kutekeleza miradi ya maji na kupunguza tatizo la maji katika maeneo yao.
Wakati
akiiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo wiki iliyopita bungeni, Waziri
wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alibainisha kuwa Wizara hiyo
imetengewa Sh bilioni 398, fedha ambazo wabunge hao walibainisha kuwa
hazitoshi, ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya maji nchini.
Wakati
akiahirisha mjadala huo wa Bajeti ya Maji, Spika alisema: “Naona sasa
mahitaji ya wabunge wote na wananchi kwa ujumla ni bajeti hii, kwa kweli
iboreshwe ili kufikia malengo stahiki katika maeneo yetu.”
Viongozi
wa Wizara ya Fedha, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Maji, kwa takribani
siku tatu, walikutana na kujadili suala hilo na namna ya kupata fedha za
kuongezea kwenye bajeti hiyo, huku wabunge wa CCM nao wakikutana ili
kuwekana sawa, kutokana na kilichotokea bungeni kuhusu bajeti hiyo.
Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alipongeza hatua za wabunge hasa
wa CCM, kuweka itikadi zao pembeni na kuungana pamoja kuikataa bajeti
hiyo, ambayo haikuwa na mfumo mzuri wa kumaliza tatizo la maji nchini.
Hata
hivyo, alipendekeza leo Serikali ije na maboresho yatakayoainisha namna
ya kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo, uliozinduliwa hivi
karibuni na Rais Jakaya Kikwete, ambao katika eneo la maji utahitaji Sh
bilioni 500.
Pamoja na mjadala wa Bajeti ya Maji kuendelea leo, pia Wizara ya Maliasili na Utalii, inatarajiwa kuwasilisha bajeti yake ya mwaka 2013/2014, itakayojadiliwa kwa siku mbili, ambapo wabunge wengi wanatarajia kuzungumzia suala la mgogoro wa ardhi Loliondo.
Bajeti ya
Wizara ya Katiba na Sheria nayo inatarajiwa kuwasilishwa kesho huku
suala la Mabaraza ya Katiba likiwa ajenda kuu, iliyopaniwa kujadiliwa
hasa na wapinzani, ambao wamekuwa wakilalamikia mchakato wake wa
uchaguzi, kwamba umekuwa ukitawaliwa zaidi na masuala ya siasa.
Katika
wiki hii, bajeti nyingine itakayojadiliwa ni ya Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambayo itajadiliwa kwa siku moja.
0 comments:
Post a Comment