Saturday, September 28, 2013

Ulimboka, Costa na Pawasa wachambua uchezaji Simba

simba_pixWACHEZAJI waliojijengea heshima kubwa wakati wakiichezea Simba wametamka maneno ya moyoni kuhusiana na mwenendo wa timu hiyo.
Wachezaji hao ni Boniface Pawasa, Victor Costa, Selemani Matola na Ulimboka Mwakingwe lakini kocha Talib Hilal alipowasikia naye akaongeza neno.
Pawasa ambaye alikuwa beki kisiki alisema: “Kikosi bado kinahitaji kurekebishwa hasa kwenye kombinesheni ya mabeki na ushambuliaji bado hapako sawa sana. Nafikiri baada ya mwaka Simba wanaweza kuwa kwenye ubora, wakizingatia misingi ya usajili, watu muhimu wakae sehemu muhimu.”
Victor Costa ambaye pia ni beki alisema: “Simba ya sasa si ya kutegemea sana kuleta mafanikio makubwa labda siku za mbele mafanikio yataonekana. Wachezaji wanahitaji muda na kuvumiliwa sana. Waachwe makocha wafanye kazi zao na pia wachezaji waliosajiliwa wapewe muda na si kuwafukuza.”
Kiungo Selemani Matola alisema: “Kikosi cha sasa ni kizuri, tena kina vijana vizuri ingawa wanahitaji kuaminiwa, watachezea timu hiyo kwa muda mrefu kwa kuwa bado ni vijana wadogo.”
Winga matata Ulimboka Mwakingwe alisema: “Sasa si kama zamani, wachezaji wengi wa sasa hawajitambui, hakuna ushindani wowote tofauti na wakati wetu tukicheza kwa kujituma na kushindania namba.
“Viongozi hawaelewi majukumu yao wengine wamekuwa wakifanya kazi ya kutafuta wachezaji wa kusajili na kuishia kusajili wasiofaa kwa kuwa hawana uelewa wa soka.
“Wamekuwa wakijipeleka nje ya nchi na kusajili vibaya, kisha wanaigharimu timu mamilioni ya fedha. Majukumu ya usajili wapewe wachezaji wa zamani kutokana na uzoefu wao,” alisisitiza Mwakingwe.
Kocha wa zamani Talib Hilal aliongeza: “Wachezaji wanatakiwa kujituma na kujiamini zaidi.”

0 comments: