Saturday, September 28, 2013

MBUNGE MSIGWA AMPONGEZA RAIS KIKWETE KWA MKAKATI WAKE WA KUPAMBANA NA UJANGILI , ASEMA YUPO TAYARI KUWATAJA WANAOTUMIA AMBULENCE KUSAFIRISHA PEMBE ZA NDOVU IRINGA

Mwenyekiti wa MANET Bw  Zuberi Mwachura  kulia  akieleza mkakati  wa  kupambana na vitendo vya ujangili katika  hifadhi ya taifa  ya  Ruaha  leo

Mbunge  wa  jimbo la  Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa akifafanua  jambo

Mgeni  rasmi  katika warsha ya  siku  moja ya  kujadili  vitendo  vya ujangili katika  hifadhi ya Taifa ya Ruaha ,mbunge  wa jimbo la Iringa mchungaji  Peter Msigwa ( wa pili kushoto) akiwa na viongozi mbali mbali akiwemo mwenyekiti wa taasisi  iliyoandaa warsha hiyo MANET Bw Zuberi Mwachura  na  viongozi  wengine
……………….
Na  Francis  Godwin Blog, Iringa
MBUNGE  wa  jimbo la  Iringa mjini kupitia chama  cha Demokrasia na maendeleo (chadema), Mchungaji Peter Msigwa amempongeza Rais  Jakaya  Kikwete kwa mkakati  wake wa kunusuru vitendo  vya ujangili  katika hifadhi  za  Taifa.
Huku  mbunge  huyo akidai  kuwa anawajua  viongozi  mbali mbali na watu maarufu ambao wanaendelea kuendesha  vitendo vya ujangili katika hifadhi ya  Ruaha  Iringa  ikiwa ni pamoja na kulitumia gari la  wagonjwa (Ambulence) kusafirisha  meno ya tembo na atawataja  wahusika  bungeni.
Msigwa  ambae ni  waziri  kivuli  wa wizara ya maliasili na utalii alitoa   pongezi  hizo  leo mjini Iringa wakati wakati akifungua kikao  cha  kujadili vitendo  vya ujangili  katika  hifadhi ya Taifa  ya  Ruaha Iringa iliyoandaliwa na taasisi  isiyo ya  kiserikali ya Mazingira Netwark Tanzania (MANET).
“Awali  ya  yote  napenda kumshukuru  sana Rais Jakaya Kikwete  kwa  kuja na mikakati ya kweli ya  kupambana na vitendo vya ujangili nchini  kwa  kutumia askari  wa jeshi la lawanchi Tanzania (JWTZ)…huu ni mkakati  mzuri ambao  binafsi  nimempongeza  sana kwa  hatua  hiyo” alisema Msigwa .
Kuwa  ni mara  kadhaa watanzania  wamepata  kusikia viongozi wa Serikali wenye dhamana wakisema kuwa mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu wa wanyamapori ni mpana na mgumu kuumaliza
Pia ni mara  kadhaa pia Serikali imeendelea kukiri kuwa mtandao huu unawahusisha Wafanyabiashara wakubwa, Wanausalama, Wabunge, Wanasiasa na watu wenye dhamana ya uongozi katika taifa letu umekuwa ni  kikwazo  kikubwa katika  vita dhidi ya ujangili.
“….Serikali imeendelea kutoa matamko kuwa itawataja wahusika wa biashara haramu dhidi ya wanyamapori na kuwachukulia hatua lakini cha kushangaza, mara zote hakuna hatua yoyote inayochukuliwa..ni jambo moja la msingi ambalo ningependa kulizungumza na kusisitiza hapa leo ni juu ya wajibu wa kila Mtanzania katika kuhakikisha kuwa tunaungana kwa pamoja katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori
Hivyo  alisema hatua ya  Rais  Kikwete  kuweka mkakati  huo wa  kutumia  askari  wa JWTZ katika kulinda  hifadhi  na kupambana na majangili  ni  jambo la kumpongeza.
Kwani  alisema baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika tamko lake maarufu mwaka 1961 lijulikanalo kama Arusha Manifesto alisema yafuatayo 
          Uhai wa wanyamapori ni jambo muhimu na linalotuhusu sana sisi sote barani Afrika. Viumbe hawa wa porini, wakiwa   katika mapori wanamoishi,sio muhimu tu kwa ajili ya       kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni sehemu ya maliasili yetu na pia ndio mustakabali wa maisha yetu ya baadaye.
Alisema  kuwa mwalimu Nyerere alitambua umuhimu wa kutunza wanyamapori kwa wakati huo tukiwa na hazina kubwa ya wanyama, lakini leo viongozi wa Serikali wameshikwa na kigugumizi katika kuhakikisha dira na jitihada za baba wa taifa letu ,vinatimizwa.
Hivyo  alisema kama kiongozi ambaye wananchi wamenipa dhamana ya kuwawakilisha, nawiwa kutumia nafasi hiyo, kuendeleza juhudi zangu na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anakua mdau nambari moja wa kupinga biashara haramu ya wanyamapori kwani si tu kuwa inalitia hasara taifa letu bali pia inaweka hatarini maisha ya wanyamapori kwa vizazi vijavyo.
Nachukua nafasi hii kuikumbusha na kuitaka Serikali kutimiza wajibu wake kwa kuwafikisha majangili na wafanyabiashara haramu wa wanyamapori katika vyombo vya dola na watendewe ipasavyo kwa mujibu wa Sheria
Kuhusu  watu  maarufu mkoani Iringa  wanaojihusisha na biashar a ya  pembe  za ndovu na hata  kutumia magari ya  umma kama Ambulence  kusafirisha pembe  hizo  za ndovu  alisema kuwa ana idadi  yao ndevu zaidi na kuwa katika kikao cha bunge  kijacho ataweka hadharani majina yao.
 Kiongozi   wa  wanaharakati  wa mtandao  wa  kupambana na vitendo vya ujangili  katika  hifadhi ya Taifa  ya  Ruaha Fundi Mihayo alisema  kuwa mbinu mbali mbali  zinatumika katika kusafirisha pembe za ndovu  ikiwa ni pamoja na usafiri  wa  boda boda kutumika  sasa  kuendeshea  vitendo  vya ujangili .
Alisema  usafiri  huo  umekuwa  ukitumika kuvushia pembe za  ndovu katika  maeneo ya vizuizi na hivyo kutaka  ulinzi  na upekuzi mkubwa unahitajika katika kukomesha vitendo  hivyo.
Kwa upande  wake mwenyekiti wa MANET Zuberi Mwachura alisema  kuwa lengo la mtandao  huo ni kuendelea  kupambana na vitendo vya ujangili  katika maeneo ya  hifadhi nchini .
Kwani  alisema  kuwa usalama wa wanyama pori na mazingira yao ni walazima kwa maendeleo yetu hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kujua na kufahamu eneo ambalo wanatoka au wanaishi watu wanao fanya au kushiriki au kujihusisha na vitendo vya ujangili ni jukumu letu kuhamasisha jamii ya wananchi wote wajione wana wajibu wa kushiliki katika vita dhidi ya ujangili. 
..lazima tukubali kwamba ujangili upo,  Pamoja na changamoto zake,  lakini hatuwezi kukaa kimya tukiacha majangili waendelee kuteketeza tembo wetu. . Mwanzo wa mafanikio katika jambo lolote ni dhamila na nidhamu, ya kupanga na kutekeleza. .. Kwa kukubaliana katika nia hii ya kupambana na ujangili ni vizuri tuwe na tamko la dhamira yetu ya kujinasua katika Lindi Kubwa la ujangili wa Tembo

0 comments: