Kocha Mkuu wa Azam, Stewart John Hall
(pichani) amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa
Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya
Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni
mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi
mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo
Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea
lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa
Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi
wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa
kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga
uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati
yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu
yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi
dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye
benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro United
inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea
lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika
Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem
Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi
kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila
ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na
kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile timu ya Azam imepigwa faini
ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na
JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam
Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia Coastal Union imetozwa faini ya
sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi
msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa
Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon imepigwa
faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha
kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal
Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka
jana.
Timu ya Burkina Faso ya Morogoro
imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya
ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24
mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia
imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao
dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage
mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya
sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia
chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh.
200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga
waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira
miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za
onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano
wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union,
JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba
Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu
baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza
kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene
baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na
washabiki.
Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni
ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na
Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya
kuchukuliwa hatua.