Friday, February 28, 2014

Real Madrid yaisulubu Schalke 04

ronaldo_8e1ea.jpg
Na Fadhy Mtanga
REAL Madrid imejihakikishia kucheza robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kuitandika Schalke 04 ya Ujerumani mabao 6-1. Mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo, mchezaji aliyevunja rekodi ya usajili ulimwenguni Gareth Bale pamoja na mchezaji mahiri Karim Benzema walihakikisha kila mmoja wao anatupia nyavuni magoli mawili ili kuifanya Real Madrid, vinara wa ligi kuu nchini Hispania, kuisulubu vilivyo Schalke 04 tena kwenda dimba lake la nyumbani, Veltins-Arena. Bao la kufutia machozi la Wajerumani hao lilifungwa na Klaas Jan Huntelaar katika dakika ya 90.
Alikuwa Karim Benzema katika dakika ya 13 tu alipopokea mpira kutoka kwa Cristiano Ronaldo na kuutumbukiza wavuni kama ishara ya ufunguzi rasmi wa karamu ya magoli ya miamba hao wa soka nchini Hispania. Kisha, panapo dakika ya 21, mchezaji aghali zaidi aliyesajiliwa kutoka Tottenham Hotspur ya Uingereza, Gareth Bale akautia mpira kimiani baada ya kupokea pasi kutoka kwa Karim Benzema.

Mwamuzi Howard Webb, anayetajwa kuwa mwamuzi bora zaidi duniani kwa sasa alipopuliza kipenga kuashiria mapumziko, Real Madrid wakarejea vyumba vya mapumziko wakiwa tayari na magoli mawili nunge.

Timu hizo ziliporejea dimbani kwa ngwe ya mwisho, ilimchukua Cristiano Ronaldo dakika saba tu kuibadili pasi kutoka kwa Gareth Bale kuwa goli la tatu. Dakika tano baadaye, dakika ya 57, Karim Benzem akafungua awali ya pili ya ufungaji kwa wasukuma ndinga hao machachari alipofunga bao la nne dhidi ya Schalke 04. Kama ilivyo kanuni ya hesabu za pythagoras, Karim alifunga goli hilo kwa kupata usaidizi kutoka kwa yule yule aliyempa pasi awali, Cristiano Ronaldo.

Dakika ya 69 ya mchezo, ikawa zamu tena ya Gareth Bale kuutia mpira wavuni baada ya kupokea pasi nzuri ya Sergio Ramos. Ubao wa matokeo ukasoma Schalke 04 0 Real Madrid 5. Matokeo hayo yalidumu kwa dakika 20 tu kwani panapo dakika ya 89 ya mchezo krosi ya Karim Benzema ikamfikia Cristiano Ronaldo. Naye hakufanya ajizi, akaitia wavuni na kuwafanya mashabiki wa Real Madrid kote ulimwenungi kushangilia kwa tambo na kujidai kwa kila namna.

Dakika iliyofuata, Klaas Jan Huntelaar aliyekuwa tayari amelimwa kadi ya njano panapo dakika ya 72, akafunga bao la kuwafutia machozi wenyeji wa mchezo huo.

Kwa matokeo hayo, Schalke 04 inahitaji miujiza ili isonge mbele. Timu hizo zinatarajia kukwaana tena katika mchezo wa pili utakaokimbizwa dimbani Santiago Bernabeu jijini Madrid, Hispania majuma matatu yajayo.

Kwingine barani Ulaya, Galatasaray iliikaribisha Chelsea, vinara wa ligi kuu ya Uingereza. Dakika ya 9 tu ya mchezo huo uliopigwa katika dimba la Turk Telekom, Fernando Torres akaifungia Chelsea goli la kuongoza. Chelsea ikawa timu ya kwanza kutoka Uingereza kufunga goli katika hatua hiyo ya 16 ya michuano ya UEFA. Timu zingine kutoka Uingereza, Machester City, Arsenal na Manchester United ziliambulia kichapo cha magoli 2-0 kutoka kwa Barcelona, Bayern Munich na Olympiakos.

Chelsea iliendelea kuongoza ikiwa ugenini hadi dakika ya 65 pale Aurelien Chedjou alipofunga akisaidiwa na Wesley Sneijer. Matokeo hayo yanaipa ahueni ya goli la ugenini Chelsea. Timu hizo zinatarajia kutimuliana vumbi tena wiki tatu zijazo pale mitaa ya Fulham, London katika dimba la Stamford Bridge.

0 comments: