Friday, September 13, 2013

RIPOTI YA (UNODC) YASEMA TANZANIA SASA NI KINARA DAWA ZA KULEVYA


*Umoja wa Mataifa wasema Tanga ni hatari
*Yaongoza Afrika Mashariki ikifuatiwa na Kenya
Na Mwandishi Wetu RIPOTI mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), imesema Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo, imesema jumla ya tani 64 za dawa za kulevya aina ya Heroine, zilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania kati ya mwaka 2010 na 2013.

Ripoti hiyo, imesema nchini Tanzania mji wa Tanga, ndio kinara na njia kuu ya kusafirishia dawa hizo kwani tangu mwaka 2010, ukamataji uliongezeka kutoka kilo 145 hadi kilo 813 mwaka huu. 

“Tanga ni njia kuu ya usafirishaji wa dawa hizi, kumekuwa na ongezeko kubwa mno tofauti na miji mingine katika ukanda wa Afrika Mashariki,” ilisema ripoti hiyo. Wastani wa ukamataji wa shehena za dawa za kulevya eneo hilo, uko katika kilogramu 1,011 mwaka 2013 kutoka 145 kilo za awali.

Takwimu zinaonyesha kwa pamoja Watanzania na Wakenya, wanaongoza kwa utumiaji na usafirishaji dawa za kulevya aina ya Cocaine, huku wakitumia dola milioni 160 kila mwaka. Lakini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kati ya mwaka 2010 na 2013, shehena zilizokamatwa na maofisa husika nchini Tanzania, Kenya, Shelisheli na Mauritius zilikuwa tani 1.6 tu. 

Takwimu hizo za kushtusha, zinatoa picha kwamba sehemu kubwa ya shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa na vyombo vya dola. Eneo la Afrika Mashariki, linaonekana kuwa kimbilio la wasafirishaji kutoka Asia hususani wa Afghanistan, Iran na Pakistan. 

Ripori hiyo, imesema Pwani ya Mashariki mwa Afrika imekuwa kitovu cha biashara na upitishaji dawa za kulevya, kwa sababu ya kukua kwa mahitaji ya ndani na kuchagizwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti dawa hizo katika eneo la Balkan, lililokuwa likiongoza kwa biashara hiyo.

Kwa mfano mwaka 2011, kilogramu 102 za dawa za kulevya zilikamatwa mjini Mombasa, lakini kufikia mwaka 2013, kiwango hicho kiliongezeka kuwa kilo 194.

Ripoti ililinganisha ukanda huo na njia ya Balkan, ambayo inaunganisha nchi za Pakistan, Iran na Uturuki kabla ya kuvusha kwenda kusini mashariki mwa Ulaya. Katika njia hiyo, ukamataji ulishuka hadi kilogramu 679 mwaka 2010, kutoka kilogramu 1,804 mwaka 2006 ikichangiwa pamoja na mambo mengine na kupungua kwa soko la Heroine barani Ulaya.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema wasafirishaji wamebuni njia nyingine ambazo bado hazijulikani kuingia Ulaya. “Mtiririko wa biashara mashariki mwa Afrika kwa hakika umeongezeka, kutokana na ukuaji wa mahitaji ya ndani au ukuaji wa matumizi katika ukanda huo kama soko au eneo la kupitisha mihadarati. 

Iwapo mashariki mwa Afrika itakuwa ‘Balkan mpya’ athari zake kwa ukanda huo, zitakuwa kubwa kama zile zilizoikumba Afrika Magharibi, ripoti ilionya.

“Hatua ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa dawa za kulevya, zinachukuliwa uzito kimataifa, lakini pia ongezeko la matumizi ndani ya mashariki mwa Afrika si jambo la kupuuza.”

Wakati dawa za kulevya zinapoondoka Afghanistan, husafirishwa kwa njia ya barabara hadi Pwani ya Makran, ukanda wa jangwani uliotambaa kutoka Pakistan hadi Iran katika mwambao wa Bahari ya Arabu na Ghuba ya Oman ambako wakazi wake wengi ni Waafrika Magharibi na Waasia.

Wasafirishaji hao wana watu wao Mashariki mwa Afrika, ambao wengi wao ni Watanzania na Wakenya wanaoendesha shughuli mpakani.

Mwaka 2011, kwa mfano, Nyakiniywa Naima Mohamed maarufu kama Mama Lela, msafirishaji maarufu wa biashara hiyo raia wa Kenya kutoka kitongoji cha Majengo mjini Nairobi, alikamatwa nchini Tanzania baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama kumtaja kuwa mmoja wa vigogo wa ‘unga’. Vigogo wa ‘unga’, hata hivyo huajiri watu wanaowabebea kutoka mataifa mbalimbali yakiwamo Waafrika Kusini na Waafrika Magharibi.

Inaelezwa wabebaji huhusika wa kusafirisha dawa za kulevya, hupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole nchini Ethiopia. Lakini imekuwa kawaida kwa Waafrika Magharibi kutumia hati za kusafiria za Afrika Kusini, wanazopata kwa njia ya kuhonga au kufunga ndoa na raia. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, baada ya Watanzania na Wakenya, raia wa Nigeria wanashika nafasi ya pili kama wabebaji maarufu zaidi, huku idadi yao kubwa wakiishi nchini Kenya. Mmoja wa Wanigeria hao, Anthony Chinedu kutimuliwa kwake nchini Kenya, kidogo kusababishe mgogoro wa kidiplomasia baina ya Kenya na Nigeria.

0 comments: