Tuesday, April 2, 2013

UKWELI KAMILI NI HUU

Na Waandishi Wetu

JENGO lenye urefu wa ghorofa 16, lililoanguka katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kusababisha vifo, ulemavu wa watu pamoja na uharibifu wa mali, lilikuwa lazima lianguke.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma Kikwete wakiwa katika wodi ya Taasisi ya Mifupa ya MOI katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam wakimpa pole kijana  Mohamed Ally Dhamji ambaye ni miongoni mwa  majeruhi walionusurika katika jengo lililoporomoka katikati ya jiji Ijumaa iliyopita na kusababisha vifo vya watu 34. (PICHA NA…

Tathmini iliyoratibiwa kisayansi na timu ya waandishi wetu, ikihusisha baadhi ya wataalamu wa majengo, inaonesha kwamba aina ya ujenzi wa jengo hilo, ulikuwa haukidhi hata kwa ghorofa tano.
Jengo lililopo jirani na lile lililoporomoka.
Machi 29, mwaka huu (Ijumaa iliyopita), jengo hilo, lililopo kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Mtaa wa Indira Ghandhi, lilianguka na kuibua wasiwasi mkubwa.
Kwa mujibu wa mhandisi wa majengo, Abel Kadali, anayemiliki kampuni yake, akiwa ni msomi mwenye shahada mbili, ujenzi wa jengo hilo, ulizungukwa na utani mwingi.
“Kwanza jengo refu kama lile linapokatika na kubomoka kisha eneo kugeuka kifusi kama hivi, maana yake ujenzi ulikuwa dhaifu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Kama ujenzi ungekuwa mzuri, hili jengo hata kama lingeanguka, lisingesambaratika kama hivi. Hapa kuna kasoro za kiweledi. Ujenzi wa namna hii, huwa unatufanya tuonekane hatuwezi kazi,” alisema.

Wananchi wakiondoa kifusi eneo la ajali.
KASORO KATIKA SARUJI
Macho ya waandishi wetu yaliona lakini Kadali akafafanua kwamba ni kosa kubwa kujenga ghorofa, halafu ukabana saruji.
“Nikishika tofali, naona ni mchanga mtupu. Kwa kadirio la kitaalamu, inaonekana kila mfuko mmoja  wa saruji, ulitengeneza matofali 90. Maana ni mchanga mtupu.
“Kwa hiyo kosa la kwanza kabisa ninaloweza kuliona hapa ni matumizi ya saruji,” alisema Kadali.

NONDO DHAIFU
Kadali alifafanua kuwa nondo zilizotumika siyo za kujengea ghorofa lenye urefu huo.
“Nikiziangalia hizi nondo, naona kabisa hili jengo lilijengwa chini ya kiwango kuanzia kwenye msingi wake mpaka hapo lilipofikia na kuanguka. Sasa ni kwa nini lisianguke?
“Tunacheza na maisha ya watu. Nondo ni nyembamba sana, nikiziangalia, zinaonesha kuwa pamoja na wembamba wake, hazina ubora,” alisema Kadali.

TATIZO LA MALIGHAFI
Kuhusu ubora wa nondo, Kadali alisema kuwa inashangaza kuona zikikunjwa zinakatika.
“Hili ni tatizo la malighafi, lazima ukaguzi wa kina ufanyike kwenye viwanda vyetu, kuona ubora wa bidhaa zinazotengenezwa.
“Ni kweli nondo ni nyembamba lakini ukweli usipindishwe kuwa hata ubora wenyewe haupo. Ina maana zilitengenezwa kwa malighafi zisizokidhi viwango.
“Viwanda vyetu vinaunda nondo kwa kuyeyusha vyuma chakavu. Ni kosa kubwa. Wakati mwingine inakuwa siyo vyuma peke yake, bali ni mchanganyiko na ‘Alminiamu’,” alisema Kadali na kuongeza:
“Kama nondo inatengenezwa kwa kuchanganya chuma na Alminiamu, unatarajia kweli kupata nondo imara? Ifahamike kwamba kila madini na kazi yake.”

KOSA LA TBS
Kadali alisema kuwa kiwango dhaifu cha nondo na bidhaa mbalimbali nchini, ni matokeo ya Shirika la Viwango Tanzania  (TBS) kutofanya kazi zake ipasavyo.
“Kuruhusu nondo kama zile kuingia sokoni na kuuzwa kwa ajili ya ujenzi, ni tatizo. TBS lazima wasimame imara kuhakikisha wanafanya kazi yao kisheria, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema Kadali.

KOSA LA NHC
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), nalo limeingia lawamani kwa sababu kisheria, lenyewe lina haki katika umiliki wa jengo hilo lililoanguka.
NHC, linamiliki asilimia 25 ya hisa za jengo hilo, hivyo kitendo cha kuacha ujenzi holela, siyo tu kwamba limeshindwa kutimiza wajibu wake, bali pia linachezea rasilimali za Watanzania.

MAITI ZAFIKIA 34
Mpaka gazeti hili linaingia mtamboni, maiti zilizokuwa zimepatikana ni 30 na jitihada za kuendelea kusaka maiti zaidi zilikuwa zinaendelea.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: “Uokoaji bado unaendelea, vyombo vyote vya dola vipo, pamoja na zana zote.”

WANANE WAKAMATWA
Kova alisema: “Mpaka sasa, polisi kanda maalum imeshawakamata watu wanane kuhusiana na kuanguka kwa ghorofa hilo.
“Waliokamatwa ndiyo waliohusika moja kwa moja, kuanzia michoro mpaka ujenzi. Kwa sasa nisingependa kuwataja majina kwa sababu uchunguzi unaendelea,” alisema Kova.
Kwa upande mwingine, Kova alisema: “Kipindi hiki tunaendelea na uokoaji, hatutarajii kupata majeruhi. Tunachofanya ni kuhakikisha tunapata maiti wote ili waweze kuzikwa kwa heshima zote kama binadamu.”

KUHUSU JENGO PACHA
Habari zinasema kuwa jengo hilo lililoanguka, lilikuwa na pacha wake, jirani kabisa na ilipo Hospitali ya Burhani. Kova amesema kuwa ujenzi wake umesimamishwa mara moja.
“Tuligundua kuwa mmiliki na mjenzi ni yuleyule, kwa hiyo tumechukua hatua za haraka sana kuzuia shughuli zote za ujenzi wa jengo hilo pacha,” alisema Kova.
Na Waandishi Wetu
JENGO lenye urefu wa ghorofa 16, lililoanguka katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kusababisha vifo, ulemavu wa watu pamoja na uharibifu wa mali, lilikuwa lazima lianguke.

0 comments: