Thursday, March 7, 2013

Ipc yalaani alichofanyiwa kibanda

0ppppppp df988
Na  Francis  Godwin,Iringa

KLABU  ya  Waandishi  wa Habari Mkoa  wa Iringa (IPC) imeeleza kusikitishwa na wimbo la vitendo vya ukatili na ukiukwaji  wa haki  za binadamu vinavyoendelea   kujitokeza  kwa  wanahabari  hapa nchini na  kulitaka  jeshi la  polisi kuusaka mtandao huu  wa utekaji wa  wanahabari nchini.Akizungumza na wanahaari mjini hapa leo , Mwenyekiti  wa IPC. Frank Leonard  alisema muda umefika kwa wanahabari nchini kote bila kujali tofauti zao kufanya tathimini ya mahusiano na wadau wao ili tahadhari zianze kuchukuliwa.

Akizungumzia tukio la  kinyama ambalo amefanyiwa  Mwenyekiti  wa  Jukwaa la  Wahariri Nchini, Absolom Kibanda ambae  pia ni Mhariri  wa Kampuni ya New Habari, Leonard alisema nimuhimu kwa wanahabari kukataa kuendelea kushuhudia wenzao wakinyamazishwa kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kuuawa.

Alisema katika mazingira ya kushangaza, ukuaji wa tasnia ya habari unaolenga kuchochea maendeleo ya nchi, unakwenda sambamba na mfululizo  wa matukio yanayolenga kuipunguza kasi hiyo.
Alisema baadhi ya wanahabari wanaofuatilia na kuchapisha au kurusha matukio yanayohusu maslai ya umma wamekuwa wakifukuzwa, wakitukanwa, wakinyang'anywa au kuvunjiwa vifaa vyao vya kazi, wakipigwa na kuuawa jambo linaouwa semokrasia, haki na maendeleo ya nchi.
"Ni wazi usalama  wa wanahabari upo mashakani; ni muhumi tukaitathimini hali hiyo na kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kupunguza mahusiano ya kudumu na  wadau  wasiopenda uwepo  wa vyombo  hivyo  vya habari," alisema.

Alisema  wakati matukio ya wanahabari kushambuliwa yakishamiri, kasi ya vyombo vya dola katika kuwasaka na kuwafikisha wahusika katika mikono ya sheria ni ndogo ikilinganishwa na matukio yanayohusu wadau wengine likiwemo jeshi la Polisi.
Leonard alisema wanahabari wanatakiwa kushikamana na kupaza sauti zao juu ili matukio ya aina hiyo yakomeshwe na yanapotokea wahusika wasakwe kwa nguvu zote na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema unyama uliofanywa kwa Kibanda, unakumbusha majonzi kwa watanzania ambao bado hawajasahau jinsi Mwandishi  wa  Channel Ten na Mwenyekiti  wa IPC, Marehemu  Daudi Mwangosi alivyouawa kinyama na Polisi wakati akitimiza wajibu wake Septemba 2, mwaka jana katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Pia  tukio la  kutekwa kwa mtangazaji  wa Redio Kwizera-Kibondo Issa Ngumba na  kukutwa akiwa ameuwawa kinyama pamoja na matukio mengine ya uvamizi  wa  wanahabari  likiwemo  la akina  Said Kubenea  na Ndimara  Tegambwage kumwagiwa  tindikali   wakiwa ofisini kwao.

"Tunajiona kama watoto tusio na msaada; kilio chetu hakifiki mbali; tuko katika wakati  mgumu tunapokuwa katika mazingira ya kutimiza wajibu wetu kwasababu hatujui nani ni adui wa habari na wanahabari," alisema.
Wakati hayo yakitokea kwa wanahabari, Leoanard alikwenda mbali zaidi na kuzungumza uwepo wa baadhi ya wanahabari wanaofurahi wakiona wanahabari wenzao wanaokutwa na matukio ya aina hiyo.
"Wapo, tena wengi tu na wengine wanajulikana; kwa lugha za mtaani wanaitwa risasi kidole, kazi yao ni kuvujisha taarifa ya kazi zinazofanywa na wanahabari wenzao kwa wadau wanaofahamiana nao; lengo lao ni kupata ujira lakini ujira unaouwa haki ya watanzania ya kupata habari zinazohusu maendeleo yao bila kujali kama ni mbaya au nzuri," alisema.
Katika kuchochea maendeleo ya taifa, Leonard alisema habari ni muhimu katika ujenzi wa Taifa; ukimfanyia unyama mwandishi wa habari unaongeza manung'uniko katika jamii na kuzorotesha maendeleo.
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kutumia nguvu zake zote kuwasaka wahusika wa tukio lililomkuta Kibanda na kuwafikisha katika vyombo vya dola ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye hila dhidi ya wanahabari na vyombo vya habari.

0 comments: