Saturday, March 29, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE AMESEMA NITAVUNJA BUNGE LA KATIBA NA KUENDELEA NA KATIBA YA ZAMANI KAMA WAJUMBE AWATAACHA FUJO




RAIS Jakaya Kikwete amesema kama mchakato wa upatikanaji Katiba Mpya utakwama kwa namna yoyote, Katiba iliyopo sasa itafanyiwa marekebisho na kuendelea kutumika.
 
Alisema kama Kiongozi Mkuu wa Serikali ni wajibu wake kuwaeleza ukweli wananchi kama alivyowasilisha hotuba yake kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba Mjini Dodoma, kuhusu hatari ya muundo wa Serikali tatu ambayo ndiyo iliyopendekezwa kwenye rasimu.
 
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi wakati akijibu risala ya wazee wa Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, waliofanya mazungumzo naye nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Subira Mgalu, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo.
 
Alisema Katiba ni jambo muhimu katika nchi na itatumika kwa miaka 50 ijayo hivyo ni wajibu wa wajumbe kupitisha Katiba bora ambayo utekelezwaji wake hautakwama baada ya kupitishwa.
 
Aliongeza kuwa, pamoja na kasoro zilizopo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba, bado hakuwasemea wajumbe wa Bunge hilo katika hotuba yake aliyoitoa bungeni bali aliamua kuweka bayana kasoro husika ili wajumbe waamue wenyewe muundo wa Serikali mbili au tatu kwani uamuzi ni wao.
 
"Mimi niliamua kutoa maoni yangu baada ya kuona Rasimu ina kasoro kwenye muundo wa Serikali tatu, sikuchukua mamlaka ya wajumbe wa Bunge hili au kuwaongoza, bali nilieleza kile ninachoamini kinaweza kutupa Katiba bora.
 
"Katiba si kwa ajili ya matumizi ya leo tu, bali kwa vizazi na vizazi, tusije kutengeneza Katiba ambayo haitekelezeki, lakini wenye maamuzi ni wajumbe wenyewe, mimi siwezi kuwatolea uamuzi lakini kama Katiba Mpya itashindwa kupatikana, hii iliyopo itafanyiwa marekebisho na mambo yataenda," alisema.
 
Akisoma risala ya wazee hao, Katibu wao Bw. Hamis Mzee, alisema wao kama wazee wanaunga mkono hotuba aliyoitoa kwa wajumbe wa Bunge hilo kwani imelenga kuwahurumia Watanzania na mzigo wanaotaka kubebeshwa na watu wachache.
 
"Sisi tunaunga mkono hatuba yako, msimamo wetu ni Serikali mbili ambazo ndizo zenye uwezo wa kuwahudumia wananchi vizuri si Serikali tatu," alisema Bw. Mzee.
 
Awali Mwenyekiti wa wazee hao, Dorothy Kihampa alisema Rais Kikwete amekuwa akiwapenda wazee na wao wanamuombea kama alivyoanza salama, basi atamaliza salama uongozi wake.
Msimamo Baraza la vyama
 
Wakati huo huo, Baraza la Vyama vya Siasa, jana limetoa tamko kuhusu mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba na kusisitiza hauridhishi kama ilivyotarajiwa na watu wengi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw. Peter Mziray alisema hali hiyo inatokana na migongano mingi inayotokea ikiongozwa na makundi ya vyama vya siasa na wanasiasa kwa nyadhifa zao tofauti.
 
"Tumekuwa tukifuatilia na kuangalia kwa makini mchakato huu na kuona wanasiasa kama wadau wakubwa wanaweza kuukwamisha kutokana na malumbano yasiyo na tija na mienendo na matendo yasiyokubalika," alisema Bw. Mziray.
 
Aliongeza kuwa, wanasiasa wamekuwa wakilalamikiwa katika mchakato huo ambapo Kamati ya Uongozi ya bara hilo, imebaini uwepo wa makundi yasiyo rasmi ndani ya Bunge hilo.
 
"Mfano wa makundi haya ni UKAWA na Tanzania Kwanza, inaonesha Bunge hili linayatambua makundi haya ambayo kimsingi kutambulika kwake, kunachochea mgawanyiko, kujenga uhasama kati ya wajumbe hivyo kudhoofisha dhana ya kufanya kazi pamoja na kufikia maridhiano.
 
"Tunatoa wito kwa wajumbe wote wa Bunge hili, kuacha kujihusisha na makundi haya badala yake wachambue na kuunga mkono hoja kwa uzito wa hoja yenyewe na kuzingatia maslahi ya Taifa badala ya kuzingatia mtazamo au msimamo wa kundi fulani," alisema Bw. Mziray.
 
Aliwataka wananchi kutambua kuwa, Bunge hilo ndio nyenzo muhimu ya kupata Katiba Mpya wanayoitaka hivyo ni vyema wakashiriki kuwahimiza wawakilishi wao watekeleze majukumu yao vizuri kwa kuepuka kufanya vitendo vya aibu na kuacha kujali masilahi binafsi bali watangulize utaifa.
 
"Kamati hii inasikitishwa na ukosefu wa nidhamu ndani ya Bunge hili jambo ambalo halikubaliki hata kwa watoto wa shule ya msingi wawapo darasani," alisema.
 
Alitoa wito kwa wajumbe wa Bunge hilo kuzingatia kanuni ambazo zinakataza vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu pamoja na kuzomea bali kila mjumbe anaweza kutoa hoja na inaweza kupingwa au kukubaliwa bila kuzomea.
 
Bw. Mziray alisema, kutokana na mwenendo wa Bunge hilo ni vyema Kamati ya Uongozi wa baraza hilo, ikutane na viongozi wote wakuu wa vyama vya siasa ambao si wajumbe wa baraza ili kushauriana na kuokoa mchakato huo.
 
Mbowe atoa lawama
Katibu wa Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo, Bw. Freeman Mbowe, ameitupia lawala sekretarieti ya Bunge Maalumu la Katiba akidai inaonekana kupokea maelekezo kutoka serikalini juu ya uendeshaji wa Bunge likiwemo suala la kubadilisha kanuni za Bunge hilo.
 
Bw. Mbowe aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ubadilishwaji wa kanuni na kuongeza kuwa, suala la kubadilisha kanuni bila ridhaa ya wajumbe ni kutengua azimio la Bunge hilo ambalo ndilo linalopitisha kanuni hizo.
 
Alisema kitendo hicho kinaashiria kutaka kulivuruga Bunge hilo ili mchakato wa kupata Katiba Mpya usifanikiwe kwani kanuni hizo zilitungwa kwa kipindi kirefu kupitia semina isipokuwa kanuni ya 37 na 38 inayoeleza aina ya upigaji kura.
 
"Aliyepewa jukumu la kubadilisha kanuni hizi ni nani, inaonekana Sekretarieti ya Bunge hili inapata maelekezo kutoka nje ya Bunge kwa maana ya serikalini, wanakaa na kuamua mambo ya Bunge hili na kutuletea, sisi UKAWA tunataka haki itendeke, hatimae kupata Katiba Mpya kwa maslahi ya wananchi," alisema.
 
Aliongeza kuwa, suala la mabadiliko ya kanuni ni jambo la msingi kwa kila mjumbe kwani wakati wa kuzipitisha kulikuwa na vikao vya mashauriano miongoni mwa pande mbili zilizokuwa zikivutana katika suala hilo hivyo kitendo cha kuzifungua kanuni hizo ni mkakati wa makusudi wenye kutaka kuleta chuki bungeni.
 
Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba alizungumzia hotuba ya Rasi Jakaya Kikwete na kusema, imesikitisha kwani hakuona umuhimu wa masuala ya Muungano na haki za wanawake.
 
Alisema Rais Kikwete alipaswa kulizindua Bunge hilo kwa kuwataka wajumbe kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Pili ili baadaye maoni hayo yapelekwe kwa wananchi lakini Rais alivunja kanuni za Bunge kwa kuhutubia masilahi ya CCM.
 
Prof. Lipumba aliongeza kuwa, UKAWA hawapo tayari kuondoka katika Bunge hilo na kuwaacha wajumbe wa CCM waandike Katiba yao kwani watakuwa wamewaangusha wananchi wanaowawakilisha ili kupata Katiba bora.

0 comments: