Thursday, February 6, 2014

Nini hatma ya kesi ya Kenyatta ICC?

KESNYATA_185c0.jpg
Pande zinazohusika katika kesi inayomkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC Mjini The Hague zimekuwa na kikao cha kujadili mstakabali wa kesi hiyo.
Kiongozi wa mashtaka wa ICC Fatou Bensouda amekiri kuwa bado hana ushahidi wa kutosha kuwezesha kesi hiyo kuendelea.
Mawakili wanaomwakilisha Rais Kenyatta wanataka kesi hiyo kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007 itupiliwe mbali.
Bensouda amesema kuwa bado kuna maswala yanayozua utata na ambayo yanahitaji uchunguzi wa kina. Viongozi wa mashitaka wanasema kuwa mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa kiasi cha kujiondoa katika kesi hiyo.
Viongozi wa mashitaka ICC wanasema kuwa Kenyatta aliongoza ghasia hizo lakini kesi dhidi yake imefanywa dhaifu kutokana na baadhi ya mashahidi kujiondoa katika kesi hiyo.
Mawakili wa Kenyatta wanatuhumu upande wa mashitaka kwa kusisitiza kutaka taarifa kuhusu akaunti ya benki ya Rais Kenyatta kuona ikiwa kuna pesa zozote zilizotolewa kwa lengo la kutumika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/08
Wakili wa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi amesisitizia mahakama kuwa kutupiliwa mbali kwa kesi kutawakosesha waathiriwa haki. Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi katika siku chache zijazo.
Rais Kenyatta alifikishwa ICC kutokana na tuhuma kuwa alikuwa mmoja wa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007/2008. Anakabiliwa na makosa ya mauaji na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.
Kadhalika Kenyatta alishitakiwa pamoja na makamu wake William Ruto kwa tuhuma sawa. Kesi dhidi ya Ruto inaendelea katika mahakama hiyo.
Watu 1,200 walipoteza maisha yao katika ghasia za uchaguzi mkuu mwaka 2007/08 huku maelfu wakilazimika kutoroka makwao. Wote wamekanusha mashitaka.
Kesi yenyewe ilitarajiwa kuanza Jumatano, lakini ikaahirishwa kwa mara ya nne mwezi jana wakati ambapo wendesha mashitaka waliposema kuwa shahidi mwingine alijiondoa kwenye kesi huku wakiomba mahakama kuwapa muda zaidi kutafuta ushahidi. CHANZO BBC SWAHILI

0 comments: