Tuesday, September 24, 2013

TIMU YA NETIBOLI YA UTUMISHI YAICHARAZA UJENZI MABAO 48-5


Timu ya Netiboli ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma kabla ya kukaguliwa kwa ajili ya mechi kati yake na timu ya netiboli ya Wizara ya Ujenzi katika viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma leo.
Timu ya Netiboli ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kabla ya kuanza mechi kati yake na Wizara ya Ujenzi katika Viwanja vya Chuo Kikuu Dodomaleo.
Timu ya Netiboli ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kukaguliwa kwa ajili ya mechi kati yake na timu ya netiboli ya Utumishi katika viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma leo.

Timu ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma ikisalimiana na timu ya Wizara ya Ujenzi kabla ya mechi leo.
Mchezaji wa Timu ya Netiboli ya Utumishi Fatma Ahmed (GS) akidaka mpira hewani  wakati wa mechi kati ya Utumishi na Wizara ya Ujenzi mjini  Dodoma leo.
Mchezaji wa timu ya Netiboli ya Utumishi Anna Msulwa (GA)(kulia) akifunga bao wakati wa mechi kati ya Utumishi na Wizara ya Ujenzi mjini Dodoma.
Mchezaji wa timu ya Netiboli ya Wizara ya Ujenzi Anjela Mvungi (GK) akidaka mpira wakati wa mechi kati ya Utumishi na Wizara ya Ujenzi mjini Dodoma.
Mchezaji wa timu ya Utumishi Joyce Mwakifamba (GD) akitoa pasi wakati wa mechi kati ya Utumishi na Wizara ya Ujenzi mjini Dodoma.
Mchezaji wa timu ya Ujenzi Bertha Wilson (GD) akitoa pasi wakati wa mechi kati ya Utumishi na Wizara ya Ujenzi mjini Dodoma.
Na Happiness Shayo – Utumishi
Timu ya Netiboli ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeendelea kufanya vizuri katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kuifunga timu ya netiboli ya Wizara ya Ujenzi mabao 48-5 katika mchezo uliofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma leo mchana.
Katika mechi hiyo,timu ya Utumishi ilionekana kuumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa kitendo kilichopelekea wachezaji wa timu ya Wizara ya Ujenzi kutokujiamini na hatimaye kupoteza mabao yao kwa wingi katika dakika ishirini za mwanzo ambapo Utumishi ilifunga mabao 12 kupitia mchezaji wake Fatma Ahmed (GS) na mengine 11 kupitia mchezaji wake Anna Msulwa (GA).
Timu ya Wizara ya Ujenzi ilitumia mbinu mbalimbali kurudisha mabao lakini ilifanikiwa kufunga bao 1 kupitia mchezaji wake Kaundime Kizaba (GA).
Kipindi cha pili cha mchezo huo Utumishi iliendelea kwa kasi ileile na kufanikiwa kuifunga timu ya Wizara ya Ujenzi mabao 25 huku Ujenzi ikifunga mabao 4.
Akiongea mara baada ya mchezo huo Kocha wa timu ya Wizara ya Ujenzi Bw.Abilai Ally alisema kuwa timu yake imejitahidi sana katika kiwango chake kwa kuwa ni timu changa.
“Mchezo ni mzuri lakini timu yetu bado ni changa kimashindano na ni mara ya kwanza kushiriki mashindano haya” alisema Bw.Ally.
Aidha,alifafanua kuwa timu hiyo ina upungufu wa wachezaji kitendo kilichopelekea kuelemewa na mchezo na kufungwa mabao mengi.
Naye mchezaji wa timu ya Utumishi Bi.Amina Ahmed (GD) alisema kuwa mchezo umeonekana mzuri kwa upande wa timu ya Utumishi kwa sababu kila mchezaji ametumia nafasi yake vizuri kwa kucheza inavyotakiwa.
Timu ya Utumishi yenye lengo la kunyakua ubingwa katika mechi zijazo imeendelea kujinoa zaidi ili kufikia lengo huku ikihakikisha haipotezi mchezo wowote katika michezo ya SHIMIWI inayoendelea mjini Dodoma.

0 comments: