Saturday, July 6, 2013

TEMEKE YALIZWA NYUMBANI MABAO 5-2 MICHUANO YA AIRTEL RISING STARS


Timu za Airtel Rising Stars zikiingia kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam tayari kwa ufunguzi rasmi wa ARS ngazi ya Taifa jana Jumanne Julai 2, 2013..

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice Singano – Mallya akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini  Dar es Salaam jana Jumanne

Mgeni rasmi Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini  Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji


Timu ya Morogoro wavulana leo Jumatano Julai 3, imeifunga timu ya Temeke 5-2 katika fainali za Taifza za Airtel Rising Stars
zinazoendelea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Morogoro waliutawala mchezo na kufanikiwa kupata magoli kupitia kwa mshambuliaji wa machachali Optatus Lupekenya ambaye alifunga magoli matatu peke yake yaani ‘hat trick’ katika dakika za 27 67 na 87.
Magoli mengine ya Morogoro yalifungwa Salum Mohamed dakika ya 72 na Evance Noshan dakika ya 80 wakati magoli ya Temeke yalifungwa na Mohamed Simba dakika ya 10 na Rajab Jumanne dakika ya 83.

Katika mchezo uliochezwa mapema asubuhi timu ya Ilala wasichana ilifanya mauaji ya kutisha baada ya kuifunga bila huruma timu ya Ruvuma 9-0 katika mchezo wa upande mmoja wa fainali za Taifa za Airtel Rising Stars. 
Mchezo huo ulionyesha wazi ya kuwa Ruvuka wanatakiwa
kufanya kazi ya ziada ili kuinua kiwango chao cha soka.

Ilala walifunga magoli yao kupitia kwa Amina Ally (dakika ya 3, 28 na 51), Donisia Daniel (dakika ya 20 na 45), Zuwena Aziz (dakika ya 23 na 35), Madeline Sylvester (dakika ya 8) na Fatuma Bahau (dakika ya 12).

Katika mchezo uliochezwa Jumanne jioni katika uwanja huo huo, timu ya  kombaini ya Mwanza (wavulana) ilitoa onyo kwa timu zinazoshiriki michuano hiyo baada ya kuifunga timu ngumu ya Ilala 3-1.

Huo ulikuwa mchezo rasmi wa ufunguzi wa Airtel Rising Stars Taifa 2013 ambapo mgeni rasmi Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Kassim Majaliwa aliwataka vijana kuonyesha vipaji vyao.

“Katika dunia ya leo mpira wa miguu ni moja ya vyanzo vya ajira vya kutumainiwa kwa vijana”, alisema Majaliwa na kuwahamasisha vijana hao kucheza kwa kujituma na kutumia mashindano ya Airtel Rising Stars kama fursa ya kuonyesha umahiri wao wa kusakata kabumbu. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice Singano alisisitiza nia thabiti ya kampuni yake kuendeleza kusaidia programu hii ya vijana.

Mchezo kati ya Mwanza na Ilala ulikuwa wa kuvutia huku timu zote zikionyesha kiwango kizuri kwa kugongeana pasi za uhakika. Mwanza walifanikiwa kupata goli la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Nassor ambaye aliwapita walinzi wa Ilala na kutia mpira wavuni. Goli hilo lilidumu hadi mapumziko.

Ilala walianza kipindi cha pili kwa nguvu na kupata goli la
kusawazisha dakika ya 50 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Omary Hassan baada ya walinzi wa Mwanza kufanya makosa nje kidogo ya eneo la hatari. Mshambuliaji Athanas Adam aliifungia Mwanza goli la pili dakika ya 69 na Kelvin Ntalale kugongelea msumari wa mwisho dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika.

0 comments: